Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Akili mnemba/bandia [Artificial Inteligence] katika uchunguzi na tiba dhidi ya magonjwa ya saratani itafungwa na kutumika ndani ya Kituo cha Umahiri wa Matibabu ya Saratani Afrika.

Kituo hicho kinatarajiwa kujengwa Dodoma, Tanzania na Taasisi ya Global Health Catalyst ya Marekani baada ya kuingia makubaliano [MoU] na Tanzania kupitia Wizara ya Afya.

Pamoja na akili bandia, kituo hicho kitatoa huduma za ubingwa bobezi wa juu zaidi za tiba ya saratani ikiwamo ‘Proton Therapy’.

Huduma hizo ndizo zinazotumika kiwango kikubwa katika ulimwengu wa sayansi ya uchunguzi na tiba dhidi ya saratani kwenye nchi zilizoendelea ikiwamo Marekani yenyewe.

Ujenzi huo unatazamiwa kuwa msaada mkubwa katika kuimarisha huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya saratani Afrika hususan nchi zilizopo Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hii ni kwa sababu, utafiti wa hivi karibuni wa Lancet unaonesha katika ukanda huo mzigo wa saratani ni mkubwa na huenda utaongezeka maradufu ifikapo 2030.

Kulingana na ripoti hiyo vifo vitokanavyo na saratani katika ukanda huu vitaongezeka maradufu kutoka 500,000 hadi Milioni moja.

“Hatuwezi tukafumba macho.., mzigo wa saratani tukiangalia Tanzania tuna wagonjwa wapya wa saratani takriban 40,000 kila mwaka,” amesema Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Ameongeza “Kila mwaka vifo ni 26,000 … wanaokufa wengi kwa saratani Tanzania ni watu maskini, wa kipato cha chini.

Amesema pamoja na kwamba takwimu za dunia zinaonesha Tanzania kuna wagonjwa wapya 40,000 lakini wanaofika hospitalini kwa mwaka ni takriban 30% tu.

“Wagonjwa wengi wa saratani wapo majumbani, katika vijiji vyetu, mitaa yetu wanashindwa kufika katika vituo vya kutoa huduma za afya kwa sababu ya umbali.

“Kwa sababu ya huduma kuwa ghali, lakini katika hawa wanaofika hospitalini habari mbaya 80% wanafika saratani ikiwa hatua ya 3 au 4 .

“Kwa hiyo inakuwa ngumu kutibika na changamoto ya kupata matokeo mazuri ya tiba,” amesema.

Amesisitiza “Hivyo, suala la saratani kwa Tanzania si tu suala la kutibu bali pia katika kuzuia, kudhibiti na kuhimiza watu kupata huduma.

Amebainisha aina za saratani zinazowatesa zaidi Watanzania 25% ni ya kizazi, 10% ya matiti, 9% ya tezidume, 6.5% ya umio la chakula, 5.8% ya utumbo mpana na saratani nyinginezo.

“Saratani Tanzania inawakumba zaidi wanawake, hata ukienda Taasisi ya Saratani Ocean Road wengi utawakuta ni wanawake,” amesema na kuongeza,

“[Wengi] wametalikiwa [wamepewa talaka na waume zao], wapo katika hali duni za maisha katika hili tunaangalia suala la usawa wa kijinsia na hali zao kiuchumi.

MoU hiyo imesainiwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu na Mkurugenzi wa GHC Prof. Wil Ngwaa mbele ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Hafla hiyo imeshuhudiwa pia na Waziri Ummy na Naibu Waziri wa Afya Hassan Hamis Hafidh, Mashujaa wa Saratani, wadau wa maendeleo na waandishi wa habari.

Akizungumza, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza GHC kwa hatua hiyo na kutoa rai kwa wadau wa maendeleo kuendelea kuipa Serikali ushirikiano ili kufikia malengo.

“Kwa kuwekeza rasilimali fedha katika  kuimarisha utafiti, kuboresha miundombinu ya afya na kuhakikisha upatikanaji matibabu sawa kwa  wagonjwa wa saratani nchini.

Ameongeza “Kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, watafiti na wataalamu wa tiba kunaweza kubadilisha taswira za huduma za matibabu ya saratani nchini.

Amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa kujenga miundombinu ya huduma za afya.

Ameishukuru Serikali ya Marekani kwa ushirikiano wao kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya nchini.

Amewashukuru wadau wa GHC na wawekezaji wa ndani wakiongozwa na Taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) pamoja na  CEO Roundtable kwa utayari walionyesha kushirikiana na Serikali. 

Rais Dk.Mwinyi amempongeza Rais Samia kwa uongozi na jitihada zake za kuimarisha ustawi wa maendeleo nchini.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement