Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Na Veronica Mrema

Kasi ya Magonjwa Yasiyoambukiza [NCD's] ikitajwa kuongezeka na kuathiri idadi kubwa ya watu nchini Tanzania na kuchangia vifo kwa zaidi ya 40% kila mwaka, gharama za matibabu ni 'kilio zaidi'.

NCD's imechangia kwa kiwango kikubwa ufukara na umaskini kwa makundi ya watu wanaougua na misiba mizito kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Magonjwa ya Moyo, Kisukari, Saratani, Shinikizo la Damu ilikuwa nadra miaka ya zamani za enzi za mababu na mabibi kuwapata vijana lakini hivi sasa si jambo geni tena, wengi wanaugua.

"Nina miaka 25 nimepata tatizo la Shinikizo la Damu, siku nilipoambiwa nilishtuka mno, sikuwahi kufikiri hata siku moja kwamba mimi kijana naweza kusumbuliwa namna hii," anasema Gloria Bryton.

Jumaa Ford ni mgonjwa wa figo anasema amefilisika uchumi wake kwa kujiuguza, alikuwa na mali nyingi lakini amelazimika kuuza vitu vyake vingi ili kumudu gharama za matibabu.

"Nimebakia na hapa ninapoishi tu, nilikuwa na magari matatu yote nimeuza, nyumba nyingine mbili nazo zote nimeuza, sasa natafuta ndugu wa kunichangia figo ili nipandikizwe, niwe na maisha mapya.

Nchini Tanzania mgonjwa mmoja wa figo huhitaji wastani wa kati ya Tsh. 200,000 hadi 300,000 kwa 'section' [awamu moja/moja] kwa huduma ya kuchuja damu 'dialysis' katika hospitali zake mbalimbali.

Kulingana na ripoti za Wizara ya Afya ni gharama kubwa mno ambazo wengi hawawezi kuzimudu, achilia mbali muda ambao humlazimu mgonjwa kukaa kwenye mashine kufanyiwa huduma hiyo.

Ni wastani wa saa nne ambazo huzitumia kwa 'section' [awamu] moja na huhitaji kufanya awamu tatu kwa kila wiki, ili kuondoshwa 'sumu' zilizojaa mwilini mwake.

"NCD's [ni] tishio kubwa tunaloona [hivi sasa ulimwenguni], Shinikizo la Damu wengi wanaumwa," anasema Dkt. Alphonsina Nanai.

Ni Msimamizi Mkuu wa Masuala ya NCD's wa Shirika la Afya Duniani [WHO - Tanzania].

Kulingana na watafiti wa masuala ya afya na magonjwa ya moyo kwa kawaida magonjwa mengi ya NCD's ikiwamo Shinikizo la Damu huwa hayaoneshi dalili za awali wazi wazi.

Dalili nyingi pia hufanana kwa ukaribu na dalili za magonjwa mengine, Dkt. Nanai anatolea mfano kwa wagonjwa wengi wa Shinikizo la Damu hupata maumivu ya kichwa.

"Shinikizo la Damu wengi wanaumwa kichwa [mtu] anahangaika anaumwa kichwa kumbe shinikizo limepanda mpaka akija kugundua anaweza kupoteza maisha," anasema.

Anaongeza "[Magonjwa ya Figo, Siko Seli na [madhara yatokanayo na] ajali [mbalimbali hususan za barabarani] na [matatizo ya] vifua [ni] kwa sasa yanaanza kuongezeka na kuwa tishio.

HALI YA TANZANIA

Idadi ya watu wanaougua Magonjwa Yasiyoambukiza inaonekana kuongezeka nchini Tanzania.

Ripoti ya Hali ya Utoaji Huduma za Afya ya mwaka 2023 ya Wizara ya Afya inaonesha kwa mara ya kwanza Tanzania imerekodi idadi kubwa ya ongezeko la wagonjwa wa Shinikizo la Damu na Kisukari.

Magonjwa hayo yameingia katika orodha ya magonjwa 10 yaliyoongoza kutesa idadi kubwa ya watu wenye umri wa miaka mitano na zaidi, Tanzania.

Ripoti hiyo imeorodhesha Shinikizo la Damu nafasi ya 4 wagonjwa ni  1,455,165 sawa na 5.6% huku Kisukari ikiwa nafasi ya 8 kwa wagonjwa 652,455 sawa na 2.5%.

AFYA KWA WOTE

Ni lengo namba tatu la Umoja wa Mataifa [UN] katika Malengo yake Endelevu [SDG's] ambapo kila nchi mwanachama anapaswa kufikia ifikapo 2030, Tanzania ikiwamo.

"Afya kwa wote inahusiana na uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu na kwenye hili, nataka niseme ndiyo 'fupa gumu' ambalo Serikali tunaendelea kupambana nalo sasa,".

Ni kauli yake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu. Tanzania ipo wapi?.., 

"Tukijilinganisha na Nchi zingine za Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kweli tupo vizuri, kufikia lengo la Afya kwa Wote," anasema.

Anafafanua "Afya kwa Wote kwanza inazungumzia uwepo wa miundombinu ya kutoa huduma za afya na tunafanya vizuri.

"Tumeona ujenzi wa hospitali, zahanati, vituo vya afya lakini pia upatikanaji wa vifaa tiba na dawa," anasema na kuongeza,

"[Lakini] wananchi kumudu gharama za matibabu, kwenye hili nataka niseme [wazi] ndiyo 'fupa' ambalo Serikali tunaendelea kupambana nalo sasa hivi.

".., la kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanapata huduma za afya bila ya kikwazo cha fedha,".

IDADI NI NDOGO

Tanzania ina idadi ya raia Milioni 61 kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Hata hivyo takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kuna mwamko mdogo watu kukata bima ya afya kabla ya kuugua, wengi hupata huduma kutoka fedha zao za mfukoni.

"Sasa hivi Watanzania ambao wanatumia bima ya afya kabla ya kuugua ni kama 8% tu, [yaani] kati ya kila Watanzania 100 ni wanane tu [ambao] wana bima ya afya," anasema Waziri Ummy.

Anaongeza "Madhara yake ni nini, ndiyo tunaona bima za afya sasa zinaelemewa kwa sababu hao wanaokata ni wachache.

"Lakini ndiyo wanaendesha sekta nzima ya afya ikiwamo hospitali binafsi na serikali," anasema.

Mkazi wa Tabata Ipyana Mwaijumba anasema ni muhimu Serikali kuendelea kuhimiza wananchi wake kukata bima ya afya lakini ni muhimu pia kuboresha upatikanaji wake kupitia vifurushi vinavyowekwa.

"Siyo mtu unakata bima halafu unaenda hospitali unakosa huduma ya kipimo fulani au dawa fulani eti kwa sababu haipo kwenye kifurushi ulichokata, ndiyo maana wengi wanarudi nyuma," anasema.

Hoja inayoungwa mkono na Fatuma Kassim anaongeza "Ni kweli kabisa, waimarishe upatikanaji wa huduma kuanzia vipimo hadi dawa tuvipate kwa bima siyo habari za kulazimika kuongeza fedha. 

MWELEKEO NI UPI?

Waziri Ummy anabainisha "Kufikia Afya kwa Wote sasa hii Serikali inajikita kuhakikisha tunaimarisha mifuko ya bima ya afya ikiwamo NHIF pamoja na [ile ya] sekta binafsi.

"Niliona wiki iliyopita bima binafsi wakitangaza bima zao, hilo ndiyo tutahamasisha ili watanzania wengi wajiunge.

"[Kimsingi] nafurahishwa na mjadala unaoendelea [kuhusu] NHIF kwa sababu lazima tufikie mahala tukubaliane kwamba bima ya afya sasa wengi wanapswa kuwa nayo kabla ya kuugua.

Anaongeza "Huwezi kuwa leo upo hospitali ndiyo unakata bima ya afya hiyo si bima ya afya kwa hiyo hata maneno yanayoendelea mimi nasema tukubaliane kama watanzania,

"Twendeni Bima Afya kwa Wote tukate wengi, wachache wakiugua sisi tutawahudumia wale wachache wanaougua.

Anasema hivi sasa wanapambana ndnai ya serikali kuboresha NHIF na sekta binafsi huku akitoa wito kwa makampuni kuanzisha vifungu au mipango mbalimbali kwa [ajili ya] Watanzania.

Akitolea mfano wa bima moja ya binafsi ambayo imeweka mpango wa Tsh. 70,000 kwmba ukikata mtu mmoja utapata OPD 300,000 kwa mwaka na kulazwa 1m kwa mwaka.

Kuhusu majadiliano waliyofikia na sekta binafsi juu ya vifurushi vipya vya NHIF anasema bado taarifa yao hajaipokea mezani kwake kwani wangali wanaichambua zaidi, watampatia na Umma utaelezwa.

Dkt. Nanai wa WHO anasema wanaufahamu vema mchakato huo wa Bima ya Afya kwa Wote kwa Tanzania,

"WHO tumeanza kutekeleza majukumu yetu tangu mwaka 1948 na mwaka jana tulifikia miaka 75 na tulichagua April 7, kila mwaka kuwa Siku ya Afya Duniani," anabainisha na kuongeza,

"Kwa mwaka huu tunafikia kilele cha sherehe hizo za miaka 75 ambapo kauli mbiu inasema Afya yako, Haki yako ambapo inasisitiza kila mtu ana haki ya kuangalia/kulinda afya yake.

Anaongeza "Tunahimiza ufanyaji mazoezi na kuzingatia msingi mzuri wa kula [kuepuka ulaji usiofaa ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza] kwa kujikita katika elimu ya afya.

"[WHO] imeshiriki kwa ukaribu [pia] tangu mwanzo [wa mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote] kwa kuandika madokezo, maelezo, mikakati ushauri na tunafahamu [hilo] linaendelea ili kukamilisha.

"Tutaendela kushirikianana Serikali kuliboresha, na kuhimiza jamii umuhimu wa kuangalia afya zetu kutibu mapema kuwa na bima ya watu wote itatusaidia katika maeneo hayo.

Anasisitiza "Ndiyo mpango wetu [SDG's] wa kufikiria bima ya kwa wote ili [watu wapate] hizi huduma [za uchunguzi na tiba dhidi ya] NCD's na [magonjwa] mengine [bila kikwazo cha fedha].

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement