moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Agenda kuu ni ukombozi wa mtoto dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza [NCD’s ] ambayo tafiti zinaonesha yanaongezeka kasi hivi sasa, Barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Msingi mzuri umewekwa kuongeza nguvu na kuchochea juhudi za kumkomboa mtoto wa Afrika ndani ya Mkutano wa kwanza wa Kimataifa [ICPPA].

Uliwaleta pamoja watafiti nguli, watunga Sera na watu wanaokabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza [NCD’s] kujadili mbinu zitakazosaidia Bara hilo.

Mkutano huo ulijumuisha washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa zaidi ya 15 duniani kwa siku tatu April 23 hadi 25, 2024 Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Julius Nyerere [JNICC], Dar es Salaam.

“Mkutano huu umekuwa na manufaa makubwa kwa Bara la Afrika,” anasema Mtafiti nguli mbobezi wa magonjwa ya damu hususan Siko Seli Barani Afrika Profesa Julie Makani.

USOGEZAJI HUDUMA

Magonjwa ya Siko Seli, Kisukari aina ya kwanza [T1D] na ya moyo ambayo yanaathriri watoto yamewekwa katika mkakati wa pamoja wa PEN-Plus.

Afrika inaweka msisitizo wa uanzishwaji wa kliniki za PEN-Plus ili kuongeza wigo wa upatikanaji huduma za uchunguzi na tiba kwenye jamii.

PEN-Plus ni mpango unaoendana sanjali na mkakati wa Shirika la Afya Duniani [WHO], kadhalika mikakati ya nchi husika ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa [UN].

UN kupitia Malengo Endelevu ya Dunia [SDG’s] umedhamiria kutokomeza NCD’s ifikapo 2030.

Mwakilishi Mkazi wa WHO – Malawi Dkt. Neema Rusibamayila anasema tofauti na nchi za Ulaya ni kwamba huko watu hugundulika mapema na kutibiwa mapema magonjwa hayo.

Anasema lakini katika nchi zinazoendelea bado kuna changamoto ya kuibua mapema wagonjwa wa NCD’s hali inayochangia wengi kupoteza maisha.

“Hivyo [ICPPA] tunaangalia nchi zetu zinazoendelea za huku Afrika tuweze kupanua huo wigo wa hizo huduma kuwa karibu zaidi na watu walipo,” anasema.

Anasema magonjwa kama Kisukari na Saratani jamii bado zinaamini ni ya watu wazima hali inayochangia watoto na vijana wanaokabiliana nayo kuchelewa kugundulika ili kupata huduma stahiki.

Anaongeza “Pia kuna magonjwa mengine watoto wanazaliwa nayo kama Siko Seli na Moyo au wanapata matatizo ya moyo kutokana na maambukizi mbalimbali waliyopata.

“Unakuta [changamoto] zote zinahitaji upasuaji au kuhudumiwa mapema. Kisukari wakipata watoto au vijana [miili yao] wanakosa insulin.

“Tiba yao inahitaji sindano ya insulin na kwa maisha [yao yote], wengine wanaugua mpaka wanafariki kwa sababu watu wanafikia watoto au vijana hawana kisukari,” anasisitiza.

Prof. Makani anasema mpango wa PEN-Plus umezingatia kuimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya NCD’s kwa kila mtoto.

“PEN-Plus kliniki ni ile watu wanaenda wanapata huduma kwa haya magonjwa matatu [ngazi ya msingi] badala ya [kulazimika] kwenda [kuzifuata kwengine katika] hospitali za rufaa.

MSINGI MZURI

Hatua hiyo inaelezwa, imeziweka nchi za Afrika kwenye nafasi/ramani nzuri katika kupambana na NCD’s ili kufikia SDG’s.

“Kwa sababu kabla ya mkutano huu ilikuwa ngumu kujua jinsi gani tutapambana na haya magonjwa.

“[Magonjwa haya] yanahitaji vipimo, dawa, [huduma za] upasuaji ilionekana kama nguvu zinahitajika kutumika nyingi kuweza kupambana na NCD’s.

“Lakini tulivyosema tuanze kupambana kidogo kidogo na haya matatu, hii inamaanisha mazimio na mipango iliyowekwa inawezekana,” anasisitiza Prof. Julie.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO-Afro), Dk Matsidiso Moeti anasema ni wakati mwafaka sasa kuweka kipaumbele katika mapambano dhidi ya NCD’s.

“Napongeza juhudi zinazofanywa na mataifa kadhaa lakini bado tuna changamoto kubwa katika NCD’s Barani Afrika.

Anasema NCD’s inagharimu maisha ikiwamo pia uchumi wa mataifa na raia hususan katika nchi zenye uchumi wa chini hivyo juhudi za makusudi lazima zifanyike.

Dkt. Moeti anaongeza “Ikiwa juhudi hazitafanyika huenda NCD’s itaongoza zaidi katika kuathiri vizazi na kugharimu uhai wa watoto kwa kuwa sababu kuu ya vifo vingi Barani Afrika ifikapo 2030.

“Kwa bahati mbaya, tumeshuhudia ongezeko la kasi la idadi ya wagonjwa wa NCD’s katika kipindi cha miongo miwili iliyopita katika Bara letu.

“Kuna ongezeko la lishe duni, magonjwa ya akili, unene kupitiliza, uchafuzi wa hali ya hewa pia,” anabainisha.

UTAFITI WA KINA

Kila nchi inaendelea kujikita na kujiimarisha pia katika eneo la tafiti zinazoangazia NCD’s kukomboa raia wake.

“Tafiti zipo na zinaendelea, zinaonesha maeneo gani yanaathiriwa [zaidi] na NCD’s katika nchi, dawa zipi zinaweza kupunguza athari au kutibu.

“[Tafiti] zimeongeza uelewa na uwezo wa jinsi gani ya kupambana na NCD’s,” anasema Prof. Julie.

Anasisitiza ndiyo maana ICPPA 2024 ni mkutano wenye manufaa makubwa kwani sasa kwa pamoja watafiti wameangazia magonjwa matatu badala ya mmoja mmoja.

Anasema watafiti wamekaa na kuongelea kwa kina zaidi kuhusu magonjwa hayo na kusisitiza,

“Kujua je tunahitaji kufanya nini, kujifunza kutoka [kwa] nchi zingine tafiti ambazo zimefanyika mbalimbali.

“[ICPPA] imesaidia kujua kwa sababu ukiona mwenzako alifanya kitu fulani, inakupa moyo kwamba inawezekana.

Anaongeza “Tunaweza kujifunza kutoka nchi jirani.., ni ile kukaa na kusema kwamba kwa mfano,

“Tanzania inaweza kusaidia msumbiji au Kenya ikasaidia Uganda ili tusitegemee tafiti au watalaamu kutoka [nchi za] nje.

“Tuwe tunaangalia wataalamu humu humu Afrika,” anasisitiza Prof. Julie.

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la umoja wa Mataifa la Masuala ya Watoto [UNICEF – Tanzania] Elke Wisch anasema ikiwa juhudi hazitachukuliwa NCD’s itazidi kugharimu uhai wa watoto wa Afrika.

“Watoto wanaathiriwa mno na NCD’s, hali si nzuri Afrika.., ikiwa hayatapewa kipaumbele yataendelea kuangamiza watoto na vijana wengi.

TANZANIA HAITAPUUZA

Ni miaka sita imesalia kufikia 2030 tathmini inaonesha bado mataifa mengi yapo nyuma mno kulikaribia au hata kulifikia lengo hilo.

“Tanzania tunaendelea kuchukua hatua na kuweka mikakati madhubuti kukabiliana na NCD’s ili pia kufikia lengo la kupunguza vifo.

“Hatuwezi kupuuza athari za NCD’s kwa sababu ni magonjwa ambayo yanatugharimu,” anasema Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu.

"Tumechukua hatua za makusudi kuwekeza katika ngazi ya huduma ya afya ya msingi ambako zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanahudhuria,” anabainisha.

Anasema kwa ushirikiano na Shirika la Kisukari Duniani na Taasisi ya Kisukari Tanzania, wamewapa mafunzo kwa watoa huduma za affya, ngazi ya msingi na kupeleka vifaa vya uchunguzi wa awali.

“Tumechukua pia hatua ya kusambaza chanjo ya HPV [inayokinga mwili wa msichana dhidi ya maambukizi ya kirusi cha Papilloma kinachosababisha saratani ya mlango wa uzazi].

“Kwa kampeni maalum tumelenga kuwafikia wasichana zaidi ya wasichana milioni 5 wenye umri wa miaka 9-14,” anabainisha na wanaendelea kuboresha huduma dhidi ya NCD’s na elimu kwa jamii.

MASHUJAA

ICPPA pia kwa mara ya kwanza uliwaleta pamoja watu wanaougua magonjwa hayo kujadili na kutoa mawazo yao wazi, wazi.

Prof. Julie anasema “Ni muhimu mno kushirikiana na watu wenye haya magonjwa.

“Kuhakikisha wanajipanga na wanakuwepo kwenye kongamano, mikutano, mijadala pili ni umuhimu wa kushirikiana.

“Kusema sisi [wataalamu, watafiti na watunga Sera] tutakaa tu kupambana na saratani au kisukari, uwezekano wa kufikia malengo ni mdogo.

“Lakini tukisema hebu tushirikiane tutafika mbali zaidi,”. ICPPA 2024 imesisitiza umuhimu wa kushirikisha watu wanaokabiliana na NCD’s katika ngazi zote.

“Kwenye tafiti, kushauri huduma zinakuwaje na kwenye kuongea na viongozi na jamii ili tuweze kwenda mbele,” anasema Prof. Julie.

UPO MWANGA

Dkt. Moeti anatoa rai kwa mataifa Barani Afrika kutekeleza kwa vitendo na kwa msisitizo wa juu mpango wa PEN-Plus ili kufikia malengo tarajiwa.

“Afrika lazima iwekeze zaidi sasa katika kushughulikia NCDs kwa rasilimali za kutosha na endelevu,” anasisitiza, 

Dkt. Neema anaongeza “.., [Lazima] kupanua wigo, tupige kelele ili tupate fedha za kukabiliana na haya, ninaona mwanga kwa sababu wamekutana watu mbalimbali.

“Serikali viongozi wa WHO kutoka ngazi zote, nchi za Afrika na makao makuu, wadau mbalimbali pia ambao wameguswa katika kutoa fedha.

“Kuna mwanga, wameona hili suala halijapigiwa kelele kiasi kinachotakiwa hivyo ni kuona namna gani tunaweza ile 'package' iweze kufikia serikali na wadau wanaotoa waweze kutoa,” anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement