Ni ‘askari’ waliojaliwa kupata maarifa lukuki ambayo kwa
kiwango kikubwa yanahitajika ndani ya jamii kwa usahihi wake na kwa wakati ili
kuijenga vema afya ya akili na ustawi imara kwa manufaa ya Taifa.
Madaktari wanao uwezo wa kuisaidia jamii kwa kuipatia elimu
sahihi hatimaye ikapata matokeo chanya na bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi
Maalum imefungua milango yake wazi kwa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania
[MEWATA] ili ishiriki bega kwa bega kuiokoa jamii.
Waziri Dkt. Dorothy Gwajima katika Mkutano Mkuu wa 21 wa
MEWATA Dar es Salaam amesema MEWATA ina nguvu kubwa na nafasi nzuri ya kuielimisha
jamii ili kutokomeza vitendo vya ukatili.
“Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda wizara hii maana yake ni
kwa ajili ya sekta zote zinazoratibu mambo ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Ameongeza “Mambo mengi tunayaona huku juu kama changamoto
watu wanauana, wanaharibiana, ukatili wa ki-jinsia [ndani ya jamii].
“Ndoa zinavunjika [kuna] migogoro, mifarakano, tunaona
watoto wa mitaani, mila kandamizi, desturi kandamizi,” amesema.
Amebainisha “Tunaona maamuzi ya jamii yatokanayo na imani
hasi, MEWATA itaenda kwenye jamii kutoa elimu.
“.., ya jinsi gani maamuzi hayo wanayoyafanya na taratibu
wanazofanya baadae ndiyo tunakutana na ‘presha’ [Shinikizo la Damu] huko na
magonjwa mengine sugu.
“UKIMWI, Kisukari, Ulemavu [na] Msongo wa mawazo unaosababisha
athari sasa [hivi] za maisha.
“Watu wanajikatili [na] wanakatili wengine, wanaishi na
ustawi mdogo wa ki-afya,” amesema.
Waziri Gwajima amesema ikiwa MEWATA watakwenda kule chini
[ngazi ya jamii] wataweza kuelimisha na hatimaye kutokomeza utaratibu huo mbovu
wa maisha unaozalisha matatizo mengi.
“MEWATA wana nafasi kubwa sana, kwa sababu hata Vitabu Vitakatifu
[vya kiimani/kidini] vinasema watu wangu wanapotea kwa kukosa maarifa.
“Lakini wanatakiwa wamshike sana elimu asiende zake ili
waweze kupona na kupata baraka sasa nani wa kupeleka [elimu] kwenye jamii?.
“.., hayo maarifa MEWATA kama wanawake madaktari wana
nafasi kubwa,” amesema na kuongeza,
“Tumewakaribisha waje ofisini kwetu, tuingie nao mkataba
tuweke mkakati, kufika kwenye jamii tukifanya hivyo, tutaifungua jamii yetu
wakaelewa kwamba kumbe ustawi wa afya zao.
Amesisitiza “Ustawi na utulivu hata katika vipato vyao,
watatulia. Ila uchumi unateketea hawafanyi maamuzi mazuri.
“Kwamba tutunze, tule vizuri hata hizi tupate huduma nzuri
za afya kwa sababu vituo vimejengwa na Serikali.
“Ni kwa sababu ya mfumo finyu wa fikra, na kukosa elimu
ambayo MEWATA wakiipeleka tutayapunguza mengi ... Wizara hii tunawakaribisha,”
amesema.
Rais wa MEWATA Dkt. Zaitun Bokhary amemshukuru Waziri Dkt.
Gwajima kwa kuwafungulia mlango na kwamba nafasi hiyo wataitumia vema kwa ajili
ya kuisaidia jamii.
“Huu ni mkutano wetu mkuu wa Chama [ambao hufanyika] kila
mwaka [mwaka huu] kauli mbiu yetu ni ‘Pioneering Women Health’.
“Kwa kuwa tunaingazia afya ya mwanamke, tuliona yeye ndiye
Waziri mwenye dhamana ya wanawake, watoto na makundi maalum aje atupe mada
inayohusiana na afya ya mwanamke.
Dkt. Zaituni ambaye pia ni Bingwa wa Upasuaji wa Watoto
Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH] ameongeza,
“[Pamoja] na changamoto ambazo anapata kwenye wizara yake.Tunashukuru
amefungua mlango kwetu MEWATA twende ofisini kwake.
“.., kushirikiana kuongelea afya ya mwanamke bila aibu kwa
uwazi kabisa. Kwa sababu inaonekana kuna changamoto nyingi wanapata wanawake
ila hazizungumzi.
“Ametufumbua macho [na] ametufungulia malango hatutailazima
damu [hii nafasi] tutakwenda ofisini kwake kuangalia namna tutakavyotangaza
hiyo eilimu na hususan maeneo ya vijijini,” amesema.
Chapisha Maoni