Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Uongozi imara kwa nafasi ya mlezi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania [MEWATA], Mke wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete ni alama nzuri isiyofutika.

MEWATA imemtunuku tuzo maalum kumtambua na kumshukuru kwa kujitoa kwa dhati kukisimamia na kukiongoza vema kwa ushauri na kumsihi aendelee kuwa mlezi wao wa kudumu.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amemkabidhi tuzo hiyo Mama Salma ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga hivi sasa.

Hayo yamejiri punde baada ya kuhitimika kwa matembezi ya hisani [MEWATA WOGGING – 2024] katika kiwanja chao huko Mbweni Dar es Salaam ambapo watajenga hospitali kubwa ya kisasa.

Hospitali hiyo ‘WELL WOMEN CENTER’ itajengwa katika kiwanja hicho ambacho Rais wa MEWATA Dkt. Zaitun Bokhary amesema kilipatikana kwa ufadhili wa Ubalozi wa Serikali ya Japan – Tanzania.

“Tulipata eneo hili kupitia kwa mlezi wetu Mama Salma ambaye ndiye alituongoza, tumedhamiria kufikia lengo la ujenzi wa WWC ili kuiunga mkono Serikali yetu kusogeza huduma bora za afya kwa jamii,”.

Ameongeza “Hospitali hii pamoja na kuhudumia wanawake na watoto pia itahudumia makundi mengine yote ndani ya jamii hadi vijana na wanaume.

Amesema wanatarajia ifikapo Desemba,2024 wawe tayari wameshaanza ujenzi wa msingi wake, kuweka na kuzindua jiwe lake la msingi.

“Tunaomba jamii yote, wadau wa maendeleo watuunge mkono katika hili kwa kutuchangia ili tufikie lengo letu ambalo ni jema kwa jamii yetu,” amesema.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali ipo tayari kushirikiana bega kwa bega na MEWATA katika mpango wake huo.

“Andikeni andiko lenu vizuri, lileteni Wizarani tunao wadau tutakaowashirikisha na fedha wanazo, ili ikiwezekana kabla ya Desemba, 2024 tuje kuzindua WWC,” amesema na kuongeza,

“Niwaahidi siku ya kuja kuzindua jiwe la msingi tutamuomba na kumualika hapa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amebainisha.

Akipokea tuzo yake Mama Salma ameipongeza MEWATA kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya kwa jamii tangu ilipoanzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

“Tuendeleze ‘moto’ ule ule [wa kwanza], endeleeni kuisaidia jamii kwa elimu kuhusu afya na uchunguzi wa afya,” amesema mlezi huyo wa kudumu wa MEWATA.

Ameitaka MEWATA ishirikiane kwa ukaribu na vyombo vya habari/waandishi wa habari kwani sekta hiyo ina nafasi kubwa na uwezo wa kufikia jamii kwa upana zaidi kupitia majukwaa yao.

“Ni muhimu wachukue taarifa zetu wakazitangaze kwa jamii na huko duniani, wajue MEWATA ipo [hai] na inaendelea kuisaidia jamii yake,” amesisitiza.

Ametoa rai kwa jamii kuendelea kujitokeza pale wataalamu wa afya wanapoitisha kampeni mbalimbali za uchunguzi wa afya ili kujua mapema hali za afya zao na kupata tiba stahiki mapema.

MEWATA tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitekeleza agenda zake kuu za kuielimisha jamii na kufanya uchunguzi hususan kwa magonjwa ya saratani ya matiti na kizazi ambazo zinazongoza kutesa wanawake.

Chama hicho pia kimekuwa kikihamasisha wasichana kujiamini na kusoma masomo ya sayansi hususan udaktari kwani miaka ya nyuma iliaminika ni fani/taaluma ya wanaume pekee lakini sivyo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement