Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

“Nina mabinti wawili, wote tayari nilishawapeleka kituo cha kutolea huduma za afya wamepatiwa chanjo ya HPV,”  amesema Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Alikuwa akizungumza katika matembezi ya hisani [MEWATA WOGGING] yaliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania [MEWATA].

Matembezi hayo yamefanyika eneo la Mbweni Dar es Salaam ambako MEWATA inatarajia kujenga hospitali kubwa ya kisasa [WELL MEWATA CENTER] ambayo inatarajiwa itatoa huduma kwa jinsi zote.

“Niwasisitize wazazi chanjo hii ya HPV imethibitika ni salama na ina ufanisi katika kusaidia kukinga dhidi ya maambukizi ya kirusi cha HPV,” amesema na kuongeza,

"Chanjo hii haina uhusiano na masuala ya uzazi wa mpango, msihofu kwamba mtakosa wajukuu,".

Amesema kirusi cha HPV ndicho husababisha saratani ya mlango/shingo ya kizazi.

Kwa mujibu wa shahidi za kisayansi kirusi hicho cha HPV hubebwa katika mwili wa mwanaume na kwamba mwanamke hupata maambukizi kwa njia ya kujamiiana.

Sayansi inaeleza ndani ya mwili wa mwanamke tangu alipopata maambukizi kirusi hicho huweza kuishi kwa miaka 10 kisha kuanza kuonesha athari zake.

Saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa zaidi ya 40% ikifuatiwa na ile ya matiti yenye zaidi ya 20%.

Wanasayansi wanaeleza ni gharama nafuu kuzuia maambukizi ya kirusi hicho kwa kupata chanjo ya HPV.

Lakini ni gharama kubwa mno kutibu mgonjwa mmoja wa saratani ya mlango/shingo ya kizazi.

Tanzania hivi sasa inatoa dozi moja pekee ya chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka 9 hadi 14.

Waziri Ummy amefafanua “Imethibitika kisayansi kwamba sasa hivi dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kabisa kumkinga msichana dhidi ya maambukizi ya kirusi cha HPV.

Amesema dozi hiyo hutolewa kwa msichana ambaye bado hajaanza kujamiiana hivyo wanaamini hao wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 wanastahili.

Ametoa rai kwa wazazi na walezi kujitokeza mapema kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma za afya ili nao wapatiwe chanjo hiyo.

Rais wa MEWATA Dkt. Zaitun Bokhary amesema tangu Chama hicho kilipoanzishwa wamejikita katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa ya saratani yanayotesa wanawake.

Amebainisha hususan saratani ya mlango/shingo ya kizazi na saratani ya matiti na kwamba wamekuwa wakifanya uchunguzi wa awali na kuwapatia matibabu kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali.

“Tangu MEWATA ilipoanzishwa tumeweza kuwaibua wanawake  73,744 wenye saratani ya kizazi na 9,337 wenye saratani ya matiti,” amesema.

Amesisitiza ni muhimu wasichana kupatiwa chanjo hiyo kwani itawasaidia kupata kinga thabiti dhidi ya saratani hiyo inayoangamiza uhai wa wanawake wengi hivi sasa duniani.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement