Na Veronica Mrema
Chanjo ya HPV ina uwezo wa kukinga dhidi ya kirusi cha HPV ambacho husababisha saratani ya mlango/shingo ya kizazi lakini haihusiani kabisa na
masuala ya uzazi wa mpango.
Jamii imehimizwa kuondoa hofu, woga na wasiwasi juu ya chanjo hiyo
kwani shahidi za ki-sayansi zimethibitisha ni salama na ina ufanisi
katika kumkinga msichana.
Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipofungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Kukweka Mipango na Mikakati ya
Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza Afrika.
Mkutano huo [ICPPA] umeandaliwa na Shirika la Afya Duniani Kanda ya
Afrika [AFRO-WHO] umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa
mbalimbali Barani humo.
“Tunaweza kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi kama
tutawapa watoto chanjo ya HPV,” amesema.
Amesisitiza “[Saratani ya mlango/shingo ya kizazi] tuugue
sisi [wanawake] ambao bado hatukupata chanjo [ya HPV].
Chanjo hiyo inatolewa kwa wasichana ambao bado hawajaanza
kujamiiana ili kuwakinga dhidi ya kirusi hicho cha HPV ambacho ndicho
husababisha saratani hiyo.
Tanzania kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwafikia wasichana
Mil. 4,841,298 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 ifikapo Desemba, 2024.
Sayansi imethibitisha dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kabisa kuupa mwili wa msichana uwezo wa kinga, dhidi ya kirusi hicho mbacho ni tishio kubwa hivi sasa duniani.
Waziri Ummy amesisitiza chanjo hiyo ni salama na kuongeza, “Chanjo
inatolewa kwa wasichana ambao hawajaanza kujamiiana.
“Kwa sababu kirusi kinatoka kwa mwanaume kuja kwa mwanamke. Tunaamini
watoto wa miaka 9 hadi 14 hawajaanza kujamiiana.
“Tunategemea miaka 15 -20 kizazi kilichokuwa na miaka 14 kwenda
mbele kisiwe na saratani kabisa Tanzania hilo jambo linawezekana,” amesisitiza.
Chapisha Maoni