moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema 

Siri mojawapo iliyojificha ndani ya desturi ya ufanyaji mazoezi, kuuchangamsha mwili wa binadamu, mara kwa mara ni kumsaidia kupata kinga dhidi ya ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la Damu. 

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu nguli ulimwenguni zinaonesha wazi kwamba, ufanyaji mazoezi husaidia kukinga magonjwa hayo kwa zaidi ya 50%.

Kisukari na Shinikizo la Damu [hususan la juu] ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo sasa yanatesa mamilioni ya watu ulimwenguni.

"Madaktari wanasema mazoezi hukinga mwili kwa zaidi ya 50% dhidi ya Kisukari na Shinikizo la Juu la Damu," amesema Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Ni mapema leo asubuhi alipozungumza mbele ya Waziri Mkuu [PM] Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa program/kampeni maalum ya mazoezi ya pamoja [Sports4All], Tanzania.

April 28,2024 PM Majaliwa alitangaza Serikali imeamua kuchagua kila siku ya jumamosi saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi ni mazoezi ya pamoja.

Barabara - Daraja la Tanzanite imeteuliwa kwa ajili ya hatua hiyo, ambapo njia hiyo itafungwa ndani ya muda huo kupisha watu wanaofanya mazoezi ya pamoja.

"Wananchi ni muhimu kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji unaofaa wa vyakula pamoja na kufanya mazoezi," amesisitiza Waziri Ummy.

Tathmini ya Wizara ya Afya Tanzania inaonesha NCD's ni magonjwa yanayoongezeka kwa kasi kwa kuwa na idadi kubw aya watu wanaohudhuria kliniki zake mbalimbali, kila mwaka.

Ripoti ya Hali ya Utoaji Huduma kwa mwaka 2023 ya Wizara hiyo inaonesha Kisukari na Shinikizo la Damu ambayo ni miongoni mwa NCD's yapo orodha ya magonjwa 10 yanayotesa wengi, Tanzania.


"Wajibu wetu kama Wizara ni kuhakikisha tunawakinga wananchi wasipate magonjwa," amesema Waziri Ummy na kusisitiza,

"Ndio maana tumeiomba Serikali kuu kupitia kwa Waziri Mkuu kufungwa kwa barabara hii ili kupisha mazoezi,".

Amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa kukubali ombi hilo na kuongoza mazoezi kwa siku ya kwanza.

Ni baada ya kutoa tamko la kufungwa kwa barabara hiyo kuanzia Taasisi ya Saratani Ocean Road [ORCI] kupitia Daraja la Tanzanite hadi katika viwanja vya Furaha. 

Ameahidi Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na vikundi vyote vya vijana vya mazoezi [jogging clubs] katika kuhimiza jambo hilo.

Akizungumza, PM Majaliwa amesema mazoezi hayo yanayoratibiwa na Wizara ya Afya ni moja ya afua iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Kama moja ya mikakati ya kuondokana na maradhi haya.., yeye mwenyewe [Rais Samia] alishiriki na kuhamasisha Watanzania kushiriki mazoezi," amesema.

Ametoa wito kwa viongozi wa Wilaya ya Kinondoni kufanya maboresho eneo la fukwe za Coco ili liwe safi na livutie watu wa rika mbalimbali.

Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo la fukwe na wote walioitikia wito wa kufanya mazoezi ya mwili.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement